Chuo cha NIT kununua ndege tatu
2 hours ago
Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM / CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kinatarajia kununua
ndege tano za mafunzo kukabili upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya anga
nchini, hasa marubani.
Ndege hizo zitanunuliwa mwakani kwa ushirikiano wa Serikali
na mkopo wa Dola za Marekani 21,250,000 ambazo ni takribani Sh bilioni 48.8 ambao
chuo hicho umepata kutoka Benki ya Dunia (WB).
Akizungumza jana wakati wa mahafali ya 34, Mkuu wa chuo
hicho, Profesa Zacharia Mganilwa, alisema mradi huo utakaoanza Februari mwakani
unalenga kukiwezesha chuo hicho kuwa kituo cha umahiri cha mafunzo ya marubani,
wahandisi wa matengenezo ya ndege na wahudumu wa ndani ya ndege.
“Sekta ya anga kwa sasa inakua kwa kasi kwa wastani wa
asilimia 12 kwa mwaka na rasilimali watu katika sekta hii ina changamoto nyingi
na kubwa.
“Tunaendelea kutoa mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya
ndege, mafunzo ya wahudumu wa ndani ya ndege na tupo katika hatua za mwisho za
maandalizi ya mafunzo ya urubani,” alisema Profesa Mganilwa.
Kwa mujibu wa Profesa Mganilwa, marubani waliopo nchini kwa
sasa ni 400 wakati mahitaji halisi ni kati ya 700 na 800.
Alisema pia mradi huo pia utahusisha ununuzi wa vifaa vya
teknolojia ya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya kufundishia kama mahanga ya
ndege, madarasa, maabara, karakana na mabweni.
Profesa Mganilwa alisema ili kuongeza uwezo wa chuo katika
mafunzo bora na ya kiwango cha kimataifa, wana makubaliano ya ushirikiano na
vyuo vikuu vya Chenyang Aerospace na Zhenhzhou vya nchini China na Shirika la
AVIC la China ambalo lina chuo kinachofundisha marubani Afrika Kusini
kinachodahili wanafunzi 200 kila mwaka.
Alisema pia wameanza utekelezaji wa mradi wa kukipandisha
hadhi kuwa chuo kikuu cha usafirishaji kwa ufadhili wa Serikali ya China ambapo
fedha zitatumika kujenga madarasa, maabara, kumbi za mihadhara, karakana,
mabweni na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Profesa Mganilwa alisema ujenzi utaanza mara baada ya
kukamilika kwa upembuzi yakinifu unaofanywa na timu ya wataalamu kutoka Chuo
Kiku cha Southwest Jiaotong cha China.
Profesa Mganilwa alisema kwa sasa chuo hicho kinatekeleza
mpango mkakati wa tatu wa miaka mitano (2016/2017 – 2020/2021) kwa lengo la
kuzalisha wataalamu katika nyanja zote za usafirishaji watakaoweza kukabiliana
na changamoto za maendeleo ya sekta hiyo na kushiriki azma ya Serikali ya kuwa
nchi ya uchumi wa viwanda.
“Tumeanza kuhuisha mitaala ya stashahada na shahada ya
uhandisi wa magari na mitambo na kuimarisha kituo cha ukaguzi wa magari ili
kupunguza ajali za barabarani na kuongeza ufanisi kwa magari ya aina zote,”
alisema.
Alisema pia wameendelea kutoa mafunzo na kuhuisha mitaala
ya stashahada, shahada na stashahada ya uzamili katika usafirishaji wa reli na
kwamba wameingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Taifa na Uchukuzi
cha Korea na Chuo cha Ufundi Stadi na Teknolojia cha Zhengzhou China.
Mkuu huyo wa chuo alisema katika kuboresha utoaji mafunzo
ya reli, hivi sasa wanataaluma wawili wanaendelea na mafunzo ya shahada za
uzamili katika uhandisi wa reli nchini Ethiopia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Naye mgeni rasmi katika mahafali hayo, Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alikitaka chuo hicho
kuhakikisha kinatoa mafunzo bora yatakayosaidia kupatikana wataalamu wa kisasa
katika sekta ya usafirishaji.
Aliwataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata
kuleta maendeleo ya kwao binafsi na taifa kwa kujiajiri au kuajiriwa.
Katika mahafali hayo, wahitimu 1,543 walitunukiwa tuzo
mbalimbali na kati yao wanawake ni 412 sawa na asilimia 27.
Weka Maoni yako Hapa
0 comments:
POST A COMMENT