MAKONDA ANUSURIKA MTEGO WA JPM | Pekua Ndani

Find Jobs In Tanzania

Breaking News
Loading...

Friday, December 21, 2018

MAKONDA ANUSURIKA MTEGO WA JPM


ANDREW MSECHU Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameukwepa mtego
wa Rais Dk. John Magufuli kuhusu hatima ya ufukwe wa Coco.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa kuanza kueleza
mikakati itakayofanyika, ikiwamo kuundeleza ufukwe huo sambamba na kujenga
mabanda kwa wafanyabiashara na vyoo vya kisasa.
Kutokana na maelezo hayo ya utangulizi, Rais Magufuli
alisema amemkwepa kwa kumuwahi kwani ilikuwa kuna uamuzi mgumu dhidi yake.
Alisema ufukwe huo wa Coco unatia aibu kwa sababu hakuna
hata choo hali ya kuwa mapato yanakusanywa kila siku.
Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam, wakati
wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la kisasa la Selander ambalo
linapita baharini.
“Nimefurahi maneno ya RC (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda) kuwa wataboresha pale Coco Beach kuliko kukaa vile kwa sababu
panatia aibu kwa jiji kama la Dar es Salaam.
“Eneo lile halina hata choo, ni lazima tuzizungumze aibu,
lakini wanakusanya mapato kila siku sasa sijui zinaenda wapi. Ukipaki gari pale
ni shilingi 2,000. Sasa hatujui hizo fedha zinaenda wapi.
“Zimeshindwa hata kujenga mabanda yanayofanana na pale ili
wananchi wakafanye biashara vizuri ili pawe mahali pa utalii.
“Sasa leo naona RC umenikwepa, umeniwahi ukasema hatua
utakazozichukua, bahati yako nzuri maana leo nilikuwa nichukue maamuzi magumu,”
alisema Rais Magufuli.
Alisema hatua ya Makonda kueleza kuhusu hatua walizochukua
katika eneo la Coco Beach imempa ahueni katika maamuzi aliyokuwa anatarajia
kuyatoa jana dhidi ya mkuu huyo wa mkoa.
MAKONDA
ALIVYORUKA KIHUNZI

Awali katika hotuba yake, Makonda alimshukuru Rais Magufuli
kwa kuhakikisha anairudisha Coco Beach kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam,
akisisitiza hatua hiyo inadhihirisha mapenzi ya dhati kwa watu wa mkoa huo.
Aliema baada ya Rais kurejesha ufukwe huo, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa alishatoa maelekezo ambayo tayari wameshakamilisha kwa kubuni
mradi wa kufanya katika eneo hilo.
“Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa, tayari
tumeyatekeleza na sasa tumekamilisha mradi wetu. Tulikuwa na mpango wa kukopa,
lakini kwa maelekezo ya Wizara ya Fedha tumeandaa maandiko ya miradi na
Serikali imetupa matumaini kwamba mradi wa kuboresha eneo hilo utapokamilika bado
tutaweza kuanzisha miradi mingine zaidi, ili daraja na barabara hiyo
litakapokamilika iweze kuwa na manufaa zaidi kwa wananchi,” alisema.
Alisema kutokana na namna mradi huo ulivyo, kukamilika kwa
daraja hilo hasa katika eneo linalounganisha barabara za maeneo kadhaa eneo la
Masaki, kutasaidia eneo la Coco Beach kufikika kwa urahisi, hivyo kurahishisha
shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
JINA
LA DARAJA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alipendekeza jina la
daraja hilo libadilishwe kutoka Daraja la Selander, akisema kama ikiwezekana
liitwe Tanzanite ili litumike kutangaza Tanzania na Jiji la Dar es Salaam.
“Dar es Salaam hivi sasa imebadilika sana, sasa inakuwa
jiji la biashara, nitaondoka Dar es Salaam ikiwa nzuri, nitaondoka sasa itakuwa
mahali pazuri pa kufanyia biashara kwa sababu miradi mingi inatekelezwa na
itabadilisha sura ya Dar es Salaam.
“Ninaamini siku moja kurudi kuitembelea Dar es Salaam
pamoja na kwamba mnaiita New Selander Bridge, lakini inawezekana likatafutiwa
jina zuri la kuitangaza Tanzania na Dar es Salaam kwa sababu Selander
itaendelea kuwepo.
“Waziri (Isack Kamwelwe),  mnaweza mkaitafutia jina zuri, mnaweza hata
mkaiita Tanzanite Bridge, ninazungumza tu sijasema liitwe hivyo.
“Bahati nzuri makazi ya mabalozi wengi wanakaa hapa karibu na
huwa wanakumbana na kero ya foleni hapa, nina uhakika watakapokuwa wanapita
wataitangaza Tanzanite… najaribu tu kupendekeza, lakini ninyi mtalifikiria ili
muone ni jina gani ambalo mtalipa daraja hili,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo, wakati akimalizia hotuba yake, Rais Magufuli
alisisitiza tena kwamba daraja la Kigamboni lilipewa jina la Daraja la Mwalimu
Nyerere kwa kuwa lilikuwa wazo la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere hivyo
mawazo yanamwelekeza daraja jipya liitwe Tanzanite.
“Kwa daraja hili hapa, mawazo yake ni Tanzanite kwa hiyo ni
vyema liitwe Tanzanite, lakini wizara inaweza kuamua kubuni jina jingine. Sasa
siyo msubiri hadi lije kupewa jina la mtu hapa,” alisema.
Alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa
kilomita 1.03 ambalo ni refu zaidi hapa nchini likifuatiwa na daraja la Rufiji
Mto Ruvuma mita 720, daraja la Nyerere mita 680, daraja la Magufuli Kilombero mita
384.
“Mradi huu utaleta manufaa mengi, utatatua kero ya foleni
kwa sababu hivi sasa nchi yetu hupoteza takribani Sh bilioni 400 kwa sababu ya
foleni, pamoja na kuboresha mandhari ya jiji letu, sasa watani zangu Wazaramo
wataamua kuja kufunga harusi kwenye daraja hili au wataenda daraja la Nyerere
au wataenda kwenye Fly over ya Mfugale (Mhandisi Patrick Mfugale).
“Mradi huu utagharimu shilingi bilioni 556.1, Serikali yetu
itatoa shilingi bilioni 49.457 na kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni
91.32 sawa na shilingi bilioni 206.643 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa
rafiki zetu wa Korea.
“Tunafahamu katika kazi yoyote ile changamoto hazikosekani.
Hata hawa marafiki zetu Wakorea wamepitia kwenye changamoto nyingi. Miaka ya
1961 tulikuwa tukilingana nao uchumi.
“Lakini wenzetu wakaamua kufunga mikanda leo wametupa
mkopo, sisi pia nina uhakika tukiamua tunaweza kuvuka vikwazo tunavyovipitia na
kujitegemea kiuchumi kama ambavyo wao wamefika, hivyo nawasihi Watanzania
tuendelee kushikamana na tuchape kazi, ili kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
Alitoa wito kwa wakandarasi wanaojenga daraja hilo
kukamilisha ndani ya muda wa miezi 30 waliopewa au kukamilisha kabla ya wakati.
“Ninafahamu Korea kuna mainjinia wazuri, hivyo nina hakika
katika kipindi hiki cha miezi 30 kuanzia Oktoba mwaka huu waliopewa wataweza
kukamilisha.
“Nitafurahi zaidi ukimaliza mapema kwa sababu sioni sababu
ya kuchelewa wakati kila kitu kipo, naomba wafanye kazi usiku na mchana,” alisema
Rais Magufuli.
Aliwataka wananchi kutumia fursa ya mradi huo kwa vijana
kuomba kazi na kujituma, mama lishe kupika katika eneo hilo na wajasiriamali
wengine kuwauzia bidhaa wanaofanya kazi katika mradi huo.
TANROADS
Akitoa maelezo ya ujenzi huo, Mkurugenzi wa Wakala wa
Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale alisema mradi huo una
lengo la kupunguza msongamano katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ukihusisha
daraja lenye urefu wa meta 1,030 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa
5.2.
Alisema mradi huo ulibuniwa mwaka 2008 baada ya kubaini
kwamba katika daraja la sasa la Selander hupitisha zaidi ya magari 60,000 kwa
siku na utagharamiwa na Jamhuri ya Korea Kusini.
Alieleza kuwa ujenzi huo utakamilika bila kuathiri nyumba
au uzio wa majengo yote yaliyopo katika eneo hilo ambazo nyingi ni za makazi na
ofisi za balozi mbalimbali nchini, japokuwa utaweza kugusa hifadhi ya barabara
katika maeneo hayo.
Alisema mradi huo ni moja ya miradi ya kipaumbele katika
Jiji la Dar es Salaam kama lilivyo Daraja la Kigamboni na utakamilika ndani ya
miezi 36 kuanzia sasa.
Mfugale alisema daraja hilo litakuwa na urefu wa kilometa
1.03 na upana wa meta 20, pia litakuwa na njia nne za magari na njia za wenda
kwa miguu kila upande kwa upana wa mita 2.5
Alisema kutakuwa na nguzo kuu tano zinazoshikilia daraja
hilo zitakazojengwa kwa zege kitaalamu kwenda chini na juu ya bahari, ambazo
zitashikilia nyaya 120 zinazobeba daraja hilo.
Alieleza kuwa daraja hilo linalotarajiwa kuishi zaidi ya
miaka 100 litaunganisha barabara za Kenyatta, Toure, Ufukoni na Barack Obama, ambazo
kwa pamoja zitaunganishwa kutoka pande zote mbili za daraja hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Mhandishi Kamwelwe alisema ujenzi wa daraja hilo utasaidia kutoa ajira kwa
Watanzania kwa mujibu wa sheria ya kazi ambayo itakuwa kwa mikataba ambapo
watalipwa na kutozwa kodi.
Alisema katika ajira nyingi za kampuni za kigeni hawapendi
kutoa mikataba iliyo wazi kwa Watanzania, lakini atasimamia kuhakikisha
wanapata mikataba na kwamba malipo yatafanyika kwa taratibu za Tanzania.

Weka Maoni yako Hapa

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT